UONGO KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA UNAO UONA MZURI KULINDA PENZI LAKO LISIVUNJIKE UNAKUPOTEZEA MAHUSIANO YAKO NA MUNGU KABISA.
Tumezoea kupuuzia vitu vidogo sana na kuona havina madhara katika wokovu wetu, tunahisi au tunafikiri kuwa ipo dhambi kubwa na ndogo, tumekuwa wakristo wazuri wa kusema habari njema za Yesu lakini matendo yetu hayafanani na ukristo wetu.
Unakutana na kaka/dada ana mahusiano ya uchumba na mwenzake, inatokea mmoja wapo akaanguka kwenye dhambi ya uzinzi sasa mwenzake anashtukia mchezo mchafu na kumuuliza huyu kijana wa kike/kiume mna mahusiano gani na yeye mbona siwaelewi? Unaweza ukaniuliza anashtukiaje wakati hakuniona na niko mbali naye sina jibu la moja kwa moja ila elewa haya mambo kwenye ulimwengu wa roho yana nguvu sana labda nikufikirishe kidogo hujawahi kumkumbuka mchumba wako.. Kabla hujamaliza hatua ya kumfikiri kichwani umpigie simu yeye anakuwa amekupigia tayari au unamtumia sms na yeye kule anakutumia yaani zinapishana kabisa mpaka wakati mwingine ya kwako inaweza ikagoma kwenda kwa ule mwingilio wa sms kati yako na yeye.
Unapokuwa umemliza hivyo anakuwa hana jibu la moja kwa moja zaidi atasema kwani vipi, kwani umeona nini, kwani kuna tatizo kuongea naye, yaani kwani zinakuwa nyingi mnooo, mwingine hawezi kuuliza kwanini sababu ya ile nidhamu ya uoga kulinda mahusiano yake yasipotee na mtu wake zaidi atajibu dah! Huyu dada/kaka ananitaka ila mi simtaki jamani ananilazimisha tu mpenzi wangu si unajua tena hawa wanaume/wanawake wengine walivyo my sweet ni ving'ang'anizi kweli hata kama umwambie sikutaki ataendelea kukusumbua tu, nakupenda sana my darling siwezi kukusaliti kamwe najiheshimu sana... Wizi mtupu!.
Hapo anakuwa tayari ameshazini naye na moyoni ana kuwa anahukumiwa kwa hilo kosa la kuzini lakini kwa ujinga wake wa kutoelewa anatenda dhambi nyingine tena ya uongo kwa kukudanganya wewe akidhani ndio suluhisho pekee la kulinda uhusiano wake na yeye, kumbe ndio anaharibu kabisa pasipo kuelewa yeye, kwanini nakwambia hivi unapokaa na dhambi bila kuitubia alafu mwenzako anapopata wasiwasi na wewe ukamdanganya maana yake bado utakuwa hujamaliza tatizo bali utakuwa umekumbatia tatizo ambalo linauwezekano mkubwa wa kuvunja uhusiano wako na yeye maana huwezi kujua kiwango cha mchumba wako cha kuomba mbele za Mungu kiko vipi, jiulize kama Mungu aliweza kuwakutanisha je atashindwa kuwatenganisha?.
Siku zote huwa napenda kuwaambia watu hivi, mtu mzuri ni yule anayeweza kukuambia ukweli japo unauma sana ni bora kuliko yule anayekudanganya ukapata furaha ya mda mfupi mwisho wake unakuja kugundua ulidanganywa inakuwa ni majuto ya milele na kilio kikubwa sana juu ya maisha yako.
Unapokuwa huru juu ya mchumba wako ni rahisi sana kukusaidia ukavuka tatizo lako linalokusumbua wewe binafsi hapa naomba unielewe; nazungumzia wale waliokoka tu maana ukiwa kwenye michanganyo ya Dunia huwezi ukanielewa nazungumzia nini hapa zaidi utaanza kuniuliza vimaswali vyako vya kwanini!! Maana ukiwa unazini na mwenzio ni ngumu na haitawezekana kujua huyo ndiye au siye.
Umeulizwa ama hujaulizwa na mwenzako na unaelewa kabisa ulizini na dada/kaka fulani ni bora ukatengeneza mazingira mazuri ya kuja kumwambia yeye kwanza kabla ya Mungu maana yake kama huwezi kuomba msamaha kwa anayeonekana kwa macho je Mungu asiyeonekana utawezaje kumwomba msamaha?
Uaminifu ni kitu bora sana kwa mwenzako na Mungu wako, haijalishi ulizidiwa ujanja na kaka/dada ukazini naye... Maana yake kuna hatua hukumsikiliza Roho wa Mungu wakati anakusemesha hatari iliyoko mbele yako.
Unapoendelea kufuga dhambi ya uongo juu ya mwenzako kujifanya mwaminifu kumbe ni Bomu linalo subiria kulipuka, hiyo dhambi itaendelea kukua na mwisho wa siku itazaa mtoto mwingine wa dhambi.
Elewa kabisa uchumba sio ndoa na unaweza ukavunjika pasipo kuwa na kipingamizi chochote mbele za Mungu zaidi ya maelezo ya kutosha juu ya mlalamikaji ama Mungu anaweza kukutenganisha na mwenzako pasipo kuelewa wewe ilikuwaje mpaka ikatokea hivyo, acha kujiaminisha ujinga ndani yako, Mungu aonaye sirini anakuona uchafu wako wote na hatakaa akubali uingie kwenye ndoa na kijana wake anayemwomba kila siku kwa uaminifu na utii wa hali juu.
Unaweza usinielewe leo ila ukikosea kuingia kwenye ndoa feki na mchumba feki utanielewa tu nilikuwa namaanisha nini hapa ila nasikitika utakuwa umechelewa sana, wakati ni sasa wa kutengeneza mahusiano yako na Mungu ili akupe mke/mme sahihi wa kuishi naye maisha yako yote hapa duniani mpaka kifo kiwatenganishe.


 

Comments